Wetangula awasuta Raila na Ruto kwa kutusiana hadharani

Kiongozi wa chama cha FORD Kenya Mheshimiwa Moses Masika Wetangula amewakemea vikali naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kile Wetangula anasema viongozi hawa wawili wamekosa heshima.

Wetangula akizungumza katika hafla moja, amesema Ruto na Raila wanapotosha wakenya kwa kurushiana cheche za maneno kila wakati wanapopanda jukwaani kuhutubia umma.

“Chenye nyinyi wawili mnajaribu kuonyesha wakenya na haswa wanarika ni kwamba matusi katika mikutano ya hadhara ndio njia mwafaka ya kuishi,” amesema Wetangula.

Seneta huyu wa Bungoma amewaomba Raila na Ruto wakomeshe tabia ya kutusiana huku akisema mapatano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila yalikuwa yakuleta maridhiano nchini na sio chuki na uhasama.

Ikumbukwe siku za hivi karibuni naibu Rais na aliyekuwa waziri mkuu wamekuwa wakirushiana cheche za maneno kufuatia sakata ya shilingi bilioni 21 za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer yalioko kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Seneta Wetangula pia amesema ufisadi umeivyonza nchi ya Kenya na kuziuliza idara zinazoshughulikia maswala ya kuibwa kwa mali ya umma ziingilie kati na kunasa wanaohusika.

“Visa vya ufisadi kwa njia yoyote ile ni adui kwa wakenya na watu wanapora mali ya umma na kupotea, kwa hivyo naiuliza idara ya kufanya upelelezi wa jinai DCI na tume ya kupambana na ufisadi EACC ziwachukulie hatua kali mafisadi,” aliongeza Wetangula.

Kiongozi huyu wa FORD Kenya amekariri kama mtu ni mwizi aitwe mwizi na uchunguzi ukikamilika awasilishwe mahakamani na kufungwa jela.

Facebook Comments