Wabunge wa ODM wamuonya Ruto dhidi ya kumtishia Raila

Wabunge wa chama cha Orange Democtratic Movement (ODM) leo jumapili wamemuonya naibu Rais William Ruto na viongozi wanaomuunga mkono dhidi ya kumtisha kiongozi wa chama chao Raila Odinga.

Wakiongozwa na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna, wabunge hao wamemtaja Ruto kama kizingiti katika vita dhidi ya ufisadi wakisema anapinga mapatano ya Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga almaarufu Handshake.

“Mapatano kati ya Rais Uhuru na mheshimiwa Raila yalikuwa ya kupunguza joto la kisiasa hapa nchini na pia kupigana na maovu kama ufisadi, sasa wafisadi wameanza kupinga mapatano hayo huku wakivifanya vita dhidi ya ufisadi kuwa uwanja wa siasa,” Alisema Sifuna katika kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Mbunge wa eneo bunge la Rongo Paul Abour naye ameonya kuwasilisha mswada bungeni wa kumng’oa Ruto mamlakani “kama atazidi kuwa kizuizi katika vita dhidi ya ufisadi”.

“Kama naibu Rais William Ruto atazidi kuwa kikwazo katika vita dhidi ya ufisadi, sisi kama viongozi tutawasilisha mswada katika bunge la kitaifa wa kumbadua Ruto kama naibu Rais,” Alisema Abour.

Katika siku za hivi karibuni, naibu Rais na viongozi wanaomuunga mkono wakiongozwa na seneta wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wamekuwa wakimtaja Raila kama mtu ambaye nia yake nikukiharibu chama tawala cha Jubilee, madai yaliyotupiliwa mbali na Raila.

Facebook Comments