Olivier Giroud atangaza kuihama Chelsea

Mshambuliaji wa timu ya Chelsea Olivier Giroud amesema ataihama klabu hii ya EPL na kuelekea Ufaransa mkataba wake utakapokamilika mwishoni mwa msimu huu kwa kile anasema ni kutopata muda wa kucheza chini ya mkufunzi Maurizio Sarri.

Tangu ujio wa mshambuliaji wa nchi ya Argentina Gonzalo Higuain mwezi Januari mwaka huu, Giroud hajaanza mechi yoyote ya kuwania ligi kuu ya Uingereza, EPL.

Giroud, na ambaye alishinda kombe la dunia mwaka jana akiwa na kikosi cha timu ya taifa la Ufaransa, alifunga magoli 33 katika mechi 73 za ligi kuu ya Ufaransa akiichezea timu ya Montpellier kabla ya kuhamia Arsenal mwaka wa 2012, na sasa ripoti kutoka ligi ya France Ligue 1 zinasema mshambuliaji huyu huenda akajiunga na klabu ya Olympique Lyonnais.

Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 33 amekuwa akitumika sana na Sarri kucheza michuano ya kuwania kombe la Europa huku akifanikiwa kutia kimiani magoli 9 katika mechi 9 alizocheza, na anaamini hawezi kujumuishwa kwenye kikosi kinachocheza ligi kuu.

The Blues wanashikilia nafasi ya 6 katika jedwali la ligi ya EPL wakijizolea pointi 57 baada ya kusakata mechi 30.

Facebook Comments