Nitauliza Mungu kwa nini hakumchukua Raila Odinga kitambo, Asema Didmus Barasa

Viongozi wanaomuunga mkono naibu Rais William Ruto wanazidi kumrushia cheche za maneno kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wakisema amekuwa mwiba katika chama tawala cha Jubilee.

Kiongozi wa hivi punde kumkashifu Raila ni mbunge wa eneo bunge la Kimilili Didmus Barasa anayesema Raila ni tapeli na popote anapoenda anaharibu mipango ya wenyeji. Anasema nia yake kwenye chama cha Jubilee ni kukisambaratisha.

Barasa akizungumza katika kikao na wanahabari bungeni, kikao kilichowaleta viongozi tofauti tofauti wanaomuunga Ruto mkono, alisema ni heri Mwenyezi Mungu angekuwa amemchukua kiongozi huyo wa ODM kitambo kwa sababu ‘Kenya haina haja naye kamwe.’

“Kama nitafika mbinguni siku moja nitamuuliza Mwenyezi Mungu kila wakati nikisoma gazeti ninaona watu wengi wamekufa na wachungaji wanasema Mungu uchukua wale wazuri, mimi nitamuuliza Mungu kwa nini hakumchukua Raila kwa sababu ni baadhi ya watu wenye hatuwahitaji hapa Kenya,” asema Barasa.

Mbunge huyu ameendelea na kumshambulia Raila akisema amesababisha vifo vya wakenya wengi akitaka kuingia mamlakani.

Barasa pia amewakashfu wabunge wa chama cha ODM akisema wanataka kuipindua serikali na wao kama Jubilee hawatakubali hilo kutendeka.

“Tunataka kuwaambia wabunge wa ODM ya kwamba tunajua mikakati yao ya kuipindua serikali na sisi ni werevu sana hatujaacha akili zetu nyumbani, tena sisi ni wanarika sio kama wao, unajua ukiwa mwanarika una akili nyingi sana? Tutahakikisha tumeilinda serikali kutokana na wale wanataka kuipindua na pia wale wanatumia vita dhidi ya ufisadi kama chombo cha kuzuia viongozi wengine kushikilia nyadhifa za uongozi,” Mheshimiwa Barasa akariri.

Facebook Comments