Mwakilishi wa wanawake Elgeyo Marakwet amuita Raila “MCHAWI”

Mwakilishi wa wanawake kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet Mheshimiwa Jane Kiptoo amemsuta kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kutaka kukisambaratisha chama tawala cha Jubilee.

Bi. Kiptoo amesema Raila ni ‘mchawi’ na hana nia nzuri kwa chama cha jubilee huku akisema mipango yake ni kumzuia naibu Rais William Ruto kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

“Mimi kama mama wa Elgeyo Marakwat ninasema huyo ‘mchawi’ anaitwa Raila Amollo Odinga alikuja katika nyumba yetu ya Jubilee ili kutugawanyisha, nataka kumwambia leo ameshindwa katika jina la yesu,” amesema Bi. Kiptoo.

Mbunge huyu wa kaunti amemtaja Raila kama mtu amelaaniwa huku akisema mapatano yake na Rais Uhuru Kenyatta almaarufu ‘Handshake‘ yalikuwa ya kuimaliza Jubilee.

“Rais Uhuru na naibu wake Ruto walichaguliwa na mungu, wewe ni nani unakuja kutuambia wewe (Raila) na Rais mko juu na wale wengine wako chini? Tunakupa wakati mchache mno na wakati wa mungu ukifika sijui utakimbilia wapi,” aliongezea Kiptoo mwenye hasira.

Mheshimiwa Jane Kiptoo ameendelea kumkemea Raila kwa sababu ya kufurushwa kwa mbunge wa Malindi Mheshimiwa Aisha Jumwa kutoka katika chama cha ODM.

“Mwanamme mzima anasema anataka kuitisha kiti cha Urais na anamfukuza mama kutoka kwa chama chake kisha anasema amuombe msamaha, kama wewe ni mwanaume kamili ungepaswa kusimama na useme umemsamehe Aisha Jumwa,” amesema Mheshimiwa Kiptoo.

Facebook Comments