Mechi za kuwania ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA Champions awamu ya 16 bora kuchezwa leo usiku

Manchester City kumenyana na Schalke 04 katika mechi ya awamu ya pili ya 16 bora kuwania ni nani ataingia robo fainali za kombe la ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA Champions leo usiku saa tano (23:00)

Usiku wa leo tarehe 12-3-2019 kunasakatwa mechi mbili za kuwania ligi ya mabingwa barani ulaya UEFA Champions majira ya saa tano usiku saa za Afrika Mashariki. Timu ya Juventus kutoka Italia itakuwa nyumbani Allianz Stadium kumenyana na timu ya Atletico Madrid kutoka Uhispania katika mkondo wa pili wa timu kumi na sita bora kutafuta ni nani ataingia robo fainali za kombe hili la UEFA Champions. Katika mkondo wa kwanza, Atletico Madrid ilimnyuka Juventus magoli 2-0 kwenye mechi iliyosakatiwa ugani Metropolitano. Juventus wanaingia kwenye mechi hii huku wakihitaji ushindi wa magoli 3-0 au zaidi ili waweze kwendelea mbele na michuano hii. Magoli kutoka kwa wachezaji Jose Gimenez na Diego Godin katika dakika ya 78 na 83 mtawalia iliwahakikishia Atletico Madrid wamevuna ushindi kutoka kwa wapinzani wao.
Bjorn Kuipers kutoka Uholanzi ndiye atakuwa mwamuzi wa hii mechi.

Kwingineko klabu ya Manchester City kutoka Uingereza itamkaribisha Schalke 04 ya Ujerumani katika uwanja wao wa nyumbani wa Etihad. Katika mkondo wa kwanza ‘The Citizens’ ilimpiga ‘S04‘ Mabao 3-2 kwenye mechi iliyosakatiwa ugani Veltins Arena na sasa Schalke 04 itahitaji ushindi wa mabao mawili kwa nunge ili kuimarisha juhudi zao za kucheza robo fainali za michuano hii ya ligi ya mabingwa barani Ulaya. Mabao ya Man City ilifungwa na wachezaji Sergio Aguero katika dakika ya 18, Leroy Sane akapachika wavuni goli la pili katika dakika ya 85 huku dakika ya 90 Raheem Sterling akaihakikishia City wamevuna ushindi. Schalke 04 ilifanikiwa kupata ushindi kutoka kwa mchezaji Nabil Bentaleb katika dakika ya 38 na 45 huku magoli yote akifunga kupitia mikwaju ya penalti. Manchester City inaingia kwenye mechi hii ikiwa na faida ya magoli matatu ya ugenini. Mwamuzi wa mechi hii atakuwa Clement Turpin kutoka Ufaransa.

RATIBA YA KESHO TAREHE 13-3-2019

Barcelona vs Lyon saa tano usiku (23:00)

Bayern Munchen vs Liverpool saa tano usiku (23:00)

Ubashiri wako ni gani katika mechi za leo na kesho?

Facebook Comments