Mechi za kufuzu AFCON 2019: Kenya kumenyana na Ghana

Timu ya Kenya ya mchezo wa soka Harambee Stars inatarajiwa kuchuana na Black Stars ya Ghana hapo kesho (Jumamosi) katika mechi ya mwisho ya kujikatia tiketi ya kucheza kombe la Afrika (AFCON) itakayochezewa ugani Ohene Gjan Sports Stadium, jijini Accra saa tatu za usiku (9pm).

Wakufunzi wa timu hizi mbili, Sébastien Migné wa Kenya na mwenzake wa Ghana Kwesi Appiah walitangaza vikosi vyao vitakavyojumuishwa kwenye mechi hii, vikosi hivi vikikosa baadhi ya wachezaji nyota, upande wa Harambee Stars Jesse Were na Michael Olunga wametemwa nje huku Asamoah Gyan wa Black Stars akichujwa. Ni wachezaji watatu (3) pekee wa Ghana wanaochezea ligi ya nyumbani walijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 24, hao wengine 21 wakiwa wanasakatia ligi za nje. Watatu hao ni mlinda lango Felix Annan, mlinzi Amos Frimpong na kiungo cha kati Kwame Bonsu.

WACHEZAJI WA KUTAZAMWA, KENYA

  1. Victor Wanyama – Wanyama ndiye nahodha wa kikosi cha Kenya na anasakata mpira wa kulipwa kwenye klabu ya Tottenham Hotspur inayocheza ligi ya Uingereza, EPL.
  2. Patrick Matasi – Matasi amekuwa mchezaji wa kutegemewa katika kikosi cha kocha Migné na anatarajiwa kuisaidia Stars kushinda.
  3. Allan Wanga – Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 33 ndiye atakayeziba pengo la Michael Olunga ambaye anauguza jeraha.
  4. Ismael Gonzalez – Hata ingawaje hajumuishwi sana katika kikosi cha Kenya, kiungo huyu wa kati anayechezea timu ya UD Las Palmas kule Uhispania, Wakenya wengi wana matumaini atacheza na kufanya vyema.
  5. Paul Were – Mashabiki wengi wa soka humu nchini wanaamini Were atakuwa muhimu katika mechii hii.

WACHEZAJI WA KUTAZAMWA, GHANA

  1. Thomas Partey – Mchezaji huyu wa klabu ya Atletico Madrid ni muhimu sana katika kikosi cha kocha Appiah.
  2. Mubarak Wakaso – Wakaso mwenye umri wa miaka 28 na anayesakatia soka ya kulipwa katika timu ya Alaves kule Uhispania, inaaminika atasaidia Black Stars kupata ushindi ikikumbukwa ameisaidia timu ya Alaves kushikilia nafasi ya 5 kwenye jedwali la La Liga.
  3. Andre Ayew – Mchezaji huyu ameonyesha umahiri wake akichezea timu ya Fenerbache kutoka Uturuki, na sasa mashabiki wa Ghana wanaamini atafanya vyema kwenye mchuano huu.
  4. Kwadwo Asamoah – Hajakuwepo katika kikosi cha Black Stars kwa muda mrefu lakini wengi wana matumaini kwa mchezaji huyu wa Inter Milan ya Italia.
  5. Jeffrey Schlupp – Schlupp ameisaidia timu yake ya Crystal Palace ya EPL huku akifunga magoli 4 na kuzalisha goli moja katika mechi 26 alizocheza, na sasa mashabiki wa soka Ghana wana imani naye kufanya vivyo hivyo hapo kesho.

KIKOSI CHA HARAMBEE STARS

Walinda lango: Patrick Matasi (St Georges, Ethiopia), Farouk Shikalo (Bandari)

Walinzi:
Erick Ouma (Vasalund, Sweden), Musa Mohammed (Nkana FC, Zambia), David Owino (Zesco, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg, South Africa), Philemon Otieno (Gor Mahia, Kenya), Benard Ochieng (Vihiga United, Kenya), Joash Onyango (Gor Mahia, Kenya)

Kiungo cha kati: Erick Johanna (IF Brommapojkarna, Sweden), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Belgium), Ismael Gonzales (UD Las Palmas B, Spain), Paul Were (Trikala, Greece), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, England), Francis Kahata (Gor Mahia, Kenya), Christopher Tangen Mbamba (Oskarshamns, Sweden), Dennis Odhiambo (Sofapaka, Kenya), Anthony Akumu (Zesco, Zambia)

Washambuliaji: Masud Juma (Al Nasr, Libya), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz), Piston Mutamba (Sofapaka).

KIKOSI CHA BLACK STARS

Walinda lango: Richard Ofori (Martizburg, South Africa), Lawrence Ati (Sochaux, France), Felix Annan (Asante Kotoko, Ghana)

Walinzi: Kwadwo Asamoah (Inter Milan, Italy) Lumor Agbenyenu ( Göztepe S.K, Turkey) Andy Yiadom (Reading Football Club, England) Amos Frimpong (Asante Kotoko, Ghana) Nuhu Kassim (1899 Hoffenheim, Germany) Nicholas Opoku (Udinese, Italy) John Boye (Metz,France) Joseph Aidoo (Genk, Belgium).

Kiungo cha kati: Andre Ayew ( Fenerbahçe S.K, Turkey) Mubarak Wakaso (Alaves, Spain) Christian Atsu (Newcastle, England) Kwame Bonsu (Asante Kotoko, Ghana), Ernest Asante ( Al Jazira, UAE), Thomas Partey (Atlético Madrid), Alhassan Wakaso ( Vitoria S.C, Portugal), Jeffery Schlupp ( Crystal Palace, England), Alfred Duncan (Sassuolo, Italy).

 Washambuliaji:  Caleb Ansah Ekuban (Trabzonspor, Turkey) Jordan Ayew (Crystal Palace) Emmanuel Boateng (Dalian Yifang, China).

Katika mkondo wa kwanza Kenya iliichapa Ghana 1-0 katika mechi iliyochezewa ugani kasarani Septemba mwaka uliopita. Harambee Stars wanaongoza kundi F wakiwa na pointi 7, moja mbele ya Black Stars wanaoshikilia nafasi ya pili na tayari Kenya ishajikatia tiketi ya kucheza michuano ya AFCON itakayoandaliwa nchini Misri tarehe 21 mwezi Juni mwaka huu. Ushindi au sare kwa Kenya itawawezesha kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi F. Harambee Stars washawasili Accra tayari kwa mchuano huu.

Facebook Comments