Mechi za kombe la UEFA Europa League zaingia awamu ya 16 bora

Usiku wa leo tarehe 7, machi 2019 kumeratibiwa kuchezwa jumla ya mechi nane za kuwania kombe la Europa. Timu ambazo zinaangaziwa sana ni Chelsea na Arsenal kutoka uingereza ambazo zitacheza nyumbani na ugenini mtawalia. Chelsea watawaalika Dynamo Kyiv kutoka Ukraine majira ya saa tano usiku saa za Afrika Mashariki. Chelsea na ambao wanajikokota katika ligi kuu ya Uingereza, wanahitaji ushindi katika mechi ya leo ili wazidishe matamanio yao ya kuibuka na taji msimu huu. ‘The Blues’ walifuzu katika awamu ya kumi na sita bora baada ya kuirarua Malmo FF magoli 3-1, kwa ujumla ambapo mechi ya kwanza katika uwanja wa nyumbani wa Malmo FF Swedbank Stadion, walipigwa na Chelsea mabao 2-1 na katika marudiano ugani Stamford Bridge Chelsea ikampa Malmo kichapo cha mbwa cha mabao 3-1. Timu ya Dynamo Kyiv nayo ilifuzu katika awamu hii ya kumi na sita bora baada ya kuwacharaza Olympiakos magoli 3-2 kwa ujumla.

Kwingineko, Klabu ya Arsenal itakuwa ugenini ugani Roazhon Park kumenyana na timu ya Rennes kutoka Ufaransa majira ya saa mbili na dakika hamsini na tano saa za Afrika Mashariki. Kikosi cha Arsenal kinaingia katika mechi hii baada ya kutoka kucheza na timu ya Totenham Hotspurs katika ligi ya EPL iliyotoka sare ya 1-1. Vijana hawa wa Unai Emery walifuzu kwenye awamu ya kumi na sita bora baada ya kuwachimba Bate Borisov magoli 3-1 kwa ujumla. Rennes nao walijikatia tiketi baada ya kuwafunga Real Betis ya Uhispania mabao 6-4.

Mechi zingine ambazo zimeratibiwa kuchezwa usiku wa leo ni kama ziofuatazo; Dinamo Zagreb watakuwa nyumbani kumenyana na Benfica, Eintracht Frankfurt waikaribishe Inter, Sevilla wacheze ugenini dhidi ya Slavia Prague huku Zenit St. Petersburg wakichuana na Villareal, mechi hizi zote zitachezwa saa tatu kasoro dakika tano saa za Afrika Mashariki. Katika ratiba nyingine ni kwamba timu ya Napoli itamkaribisha FC Red Bull Salzburg huku Valencia wakikaribishwa na FC Krasnodar, mechi hizi zitachezwa saa tano usiku saa za Afrika Mashariki.

Facebook Comments