Manchester United yabaduliwa FA, Manchester City ikiponea

Wachezaji wa timu ya Wolverhampton Wanderers wakisherehekea baada ya kujikatia tiketi ya kucheza nusu fainali za michuano ya kombe la FA kwa kumpiga Manchester United 2-1

Robo fainali za michuano ya kuwania kombe la The Emirates FA zilichezwa siku ya Jumamosi huku mechi tatu zikisakatwa na moja iliyosalia ikiratibiwa leo Jumapili. Manchester United walipiga dhidi ya Wolverhampton Wanderers ugani Molineux Stadium huku majirani wao Manchester City wakimenyena na Swansea City uwanjani Liberty Stadium. Red Devils walipigwa magoli 2-1 na kutupwa nje ya michuano hii, mabao ya Wolverhampton Wanderers yakifungwa na Raul Jimenez na Diogo Jota dakika ya 70 na 76 mtawalia. Bao la kufutia machozi la Man United ilitiwa kimiani na Marcus Rashford kunako dakika ya 90.

The Citizens walitoka nyuma na kushinda mabao 3-2, katika kipindi cha kwanza Swansea City ilikuwa imeongoza magoli 2-0 kupitia kwa wachezaji Matt Grimes kunako dakika ya 20 kwa njia ya penalti naye Bersant Celina akatia kimiani bao la pili dakika ya 29. Manchester City walimiliki mpira katika kipindi cha pili na kunako dakika ya 69 Bernardo Silva akafunga bao la kwanza. The Citizens walitia presha na dakika ya 78 mchezaji wa Swansea Kristoffer Nordfeldt akajifunga na kufanya mambo kuwa 2-2. Nguvu mpya Sergio Aguero alifunga bao la tatu katika dakika ya 88 na kuihakikishia Man City kucheza nusu fainali za michuano ya FA.

MATOKEO YA FA JUMAMOSI

Watford 2-1 Crystal Palace

Swansea City 2-3 Manchester City

Wolverhampton Wanderers 2-1 Manchester United

Watford, Manchester City na Wolves wanangoja droo ya nusu fainali itakayotolewa leo jumapili baada ya kukamilika kwa mechi kati ya Millwall na Brighton & Hove Albion.

Nusu fainali za michuano hii ya FA zitachezwa Aprili 6 huku fainali ikipigwa tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu wa 2019.

Facebook Comments