Liverpool yaponea, Chelsea ikichukua pointi 3 muhimu mikononi mwa Cardiff

Michuano ya kuwania ligi kuu ya Uingereza, EPL imeendelea leo huku jumla ya mechi mbili zikisakatwa. Klabu ya Liverpool imeponea mikononi mwa Tottenham Hotspur katika kipute kikali kilichosakatiwa ugani Anfield huku bao la ushindi la ‘The Reds‘ likifungwa na mchezaji wa Spurs katika dakika za mwisho. Mechi nyingine ilikuwa kati ya Chelsea na Cardiff City ugani Cardiff City Stadium ambapo ‘The Blues‘ imevuna ushindi.

Katika mechi ya Liverpool na Tottenham Hotspur, ‘The Reds’ imemlima Spurs magoli 2-1 huku mabao hayo mawili yakitiwa kimiani na wachezaji Roberto Firmino kunako dakika ya 16 naye mchezaji wa spurs Toby Alderweireld akajitinga bao katika dakika ya 90 na kuihakikishia Liverpool ushindi. Bao la kufutia machozi la vijana wa Spurs limefungwa katika dakika ya 76 na Lucas Moura.

Kwingineko Chelsea imetoka nyuma na kujinyakulia pointi tatu kwa kuifunga Cardiff City mabao 2-1, magoli ya ‘The Blues‘ yakifungwa na wachezaji Cesar Azpilicueta na Loftus Cheek katika dakika ya 61 na 90 mtawalia huku bao la Cardiff likitiwa kimiani na Victor Camarasa kunako dakika ya 46.

Kwa sasa Liverpool ndiyo inaongoza katika jedwali la ligi kuu ya EPL ikiwa na pointi 79, pointi mbili mbele ya Manchester City huku ‘The Reds‘ ikiwa imecheza mechi 32 nayo ‘Citizens‘ 31. Tottenham Hotspur inashikilia nafasi ya tatu ikijizolea pointi 61, pointi sawia na Manchester United inayoridhika na nafasi ya nne huku Arsenal na Chelsea wakijizolea pointi 60, ‘The Gunners‘ ikishikilia nafasi ya 5.

Facebook Comments