Liverpool, Barcelona waingia robo fainali za ligi ya mabingwa barani ulaya

Mchezaji wa Liverpool Sadio Mane aungana na wenzake kushangilia baada ya kufunga bao la tatu dhidi ya Bayern Munchen katika mechi ya kuwania ni nani atacheza robo fainali za ligi ya mabingwa barani ulaya, UEFA Champions. Liverpool ilishinda kwa magoli 3-1.

Mechi za awamu ya kumi na sita bora za ligi ya mabingwa barani ulaya mkondo wa pili zilikamilika jana huku timu nne zikijimwaya uwanjani. Klabu ya Liverpool kutoka Uingereza ilicharaza Bayern Munchen ya Ujerumani mabao 3-1 katika kipute kikali kilichosakatiwa ugani Allianz Arena. Magoli ya Liverpool yalitiwa kimiani na wachezaji Sadio Mane dakika ya 26, Virgil Van Dijk akafunga bao la pili katika dakika ya 69 na kisha Sadio Mane akawahakikishia Liverpool kucheza robo fainali za UEFA Champions kwa kufunga goli la tatu dakika ya 84. Bao la kufutia machozi la Bayern lilifungwa na mchezaji wa Liverpool Joel Matip alipochanganyikiwa na kujifunga kunako dakika ya 39. ‘The Reds’ walikuwa wanahitaji ushindi au sare ya kufungana magoli yoyote ikikumbukwa katika mkondo wa kwanza walitoka sare tasa ugani Anfield.

Kwingineko Barcelona iliwatinga Lyon ya Ufaransa magoli 5-1 katika mechi iliyochezewa ugani Nou Camp. Mabao ya ‘Barca’ yalifungwa na wachezaji Lionel Messi katika dakika ya 18 kwa njia ya penalti, Philippe Coutinho akaweka la pili kunako dakika ya 31, Lionel Messi akaongeza la tatu dakika ya 78, Dakika ya 81 Gerard Pique akafunga la nne na kisha Ousmane Dembele akafanya mambo kuwa 5-1 dakika ya 85. Goli la Lyon lilifungwa na Lucas Tousart kunako dakika ya 58.

Sasa timu za Liverpool na Barcelona zinangoja droo ya robo fainali za kombe hili la mabingwa litakalofanywa Ijumaa hii ya tarehe 15 kwenye makao makuu ya UEFA jijini Nyon, Uswisi. Timu zilizoingia katika robo fainali hii ni 8 huku nne zikitokea Uingereza, nazo ni; Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur. Timu zingine ni pamoja na Barcelona ya Uhispania, Juventus kutoka Italia, Ajax ya Uholanzi na klabu ya Porto kutoka Ureno.Facebook Comments