Gor Mahia yavuna ushindi mnono, Leopards ikilazimishwa sare na Vihiga United

Klabu ya Gor Mahia imepanda hadi nafasi ya pili katika jedwali la ligi kuu nchini, KPL baada ya kuwacharaza Zoo Kericho magoli 4-0, kwa sasa K’Ogalo ina pointi 35 pointi moja nyuma ya viongozi Sofapaka ambao wamecheza mechi 19 huku Gor Mahia ikisakata 16.

Mabao ya K’Ogalo yalifungwa na wachezaji Kenneth Muguna aliyefungua ukurasa kunako dakika ya 18, Dakika mbili baadae Dennis Oliech akaongeza la pili, Nicholas Kipkirui akatia kimiani la tatu dakika ya 81, na kisha Oliech akafunga la nne katika dakika ya 82.

Kwingineko Sofapaka iliendelea kushikilia nafasi ya kwanza kwa kuiridima Mount Kenya United mabao 3-1 katika kipute kilichosakatiwa ugani Kenyatta Stadium, kaunti ya Machakos.

Magoli ya Batoto ba Mungu yalitiwa wavuni na wachezaji Stephen Waruru katika dakika ya 4 naye Micheal Oduor akafunga la pili na la tatu kunako dakika ya 63 na 65 mtawalia.

Vijana wa Sam Timbe walionekana kutawala mchuano baada ya Mt. Kenya United kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 79, hata hivyo, walipata bao la kufutia machozi dakika ya 28 kwa hisani ya Joseph Wanyonyi.

MATOKEO YA KPL, JUMATANO

Kenya CB 1-1 Western Stima

Bandari 1-2 Kakamega Homeboyz

Tusker 3-1 Kariobangi Sharks

Ulinzi Stars 2-1 Sony Sugar

Vihiga United 2-2 AFC Leopards

Zoo Kericho 0-4 Gor Mahia

Sofapaka 3-1 Mount Kenya United

JEDWALI LA LIGI YA KPL

Facebook Comments