Gor Mahia yaandikisha historia kwa kuwa timu ya Kwanza kutoka Kenya kuingia robo fainali za CAF

Wachezaji wa Gor Mahia wakisherehekea baada ya kujikatia tiketi ya kucheza robo fainali za michuano ya CAF Confederation kwa kuwapiga Petro Atletico goli 1-0 katika mechi iliyosakatiwa ugani Kasarani Stadium, Nairobi

Klabu ya Gor Mahia inayocheza ligi kuu nchini KPL jana (Jumapili) ilijikatia tiketi ya kucheza robo fainali za michuano ya kuwania kombe la CAF Confederation baada ya kuinyuka Petro Atletico ya Angola goli 1-0 kupitia kwa mchezaji Jacques Tuyisenge aliyefunga kwa njia ya Penalti kunako dakika ya 58.

Mchuano huu ulichezewa ugani Kasarani Stadium jijini Nairobi, kufuatia ushindi huo wa mechi za kundi D, K’Ogalo iliandikisha historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka nchini Kenya kucheza robo fainali za mechi hizi.

Ni mchezo uliojawa na vituko kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho na kupelekea wachezaji wawili wa Gor Mahia kuonyeshwa kadi nyekundu na pia makocha wote wa timu hizi wakafurushwa uwanjani.

Wachezaji wa K’Ogalo Ernest Wendo na Shafiq Batambuze walitimuliwa uwanjani dakika ya 36 na 76 mtawalia, Wendo alimchezea visivyo Vladamir Eston wa Petro huku Batambuze akionyeshwa kadi mbili za manjano naye mkufunzi wao Hassan Oktay akitimuliwa dakika ya 10 kwa kumrushia cheche za maneno mwamuzi wa mechi hio.

Gor Mahia walimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi D wakijizolea pointi 9 sawia na viongozi Zamalek tofauti ikiwa ni magoli tu.

Robo fainali hizi zitachezwa kati ya tarehe 5 na 12 mwezi Mei mwaka huu wa 2019.

Facebook Comments