Baba amuua bintiye wa miaka 6, Mutomo-Kitui

Baba amuua bintiye wa miaka 6 katika kijiji cha Muthingitho huko Mutomo kaunti ya Kitui.

Msichana mwenye umri wa miaka sita anadaiwa kuchinjwa na babake usiku wa kuamukia leo (Jumamosi) katika kijiji cha Muthingitho kwenye kata ya Kibwea ilioko Mutomo kaunti ya Kitui.

Kulingana na kaimu kamishena wa Mutomo Bwana Jacob Ouma, mwanamme huyo ambaye ametambuliwa kama Mutinda Masila alimuua mwanawe Mbuli Mutinda kwa kumchinja akitumia kisu.

Ouma amesema mshukiwa alitekeleza unyama huo kwa mtoto wake aliyekuwa akisoma darasa la kwanza kwenye shule ya msingi ya Kisayani baada ya ugomvi na mkewe.

Baada ya kumuua bintiye, Mutinda anasemekana alijificha katika mlima mmoja eneo hilo huku maafisa wa polisi wakimsaka naye akitishia kujitoa uhai.

Hata hivyo, Bwana Ouma amedhibitisha baba huyo katili alijitia kitanzi kwa kujirusha kutoka kwa mlima aliokuwa amejificha huku mwili wake ukihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Mutomo.

Facebook Comments