Arsenal yapigwa, Chelsea ikishinda katika mechi za 16 bora za Ligi ya Europa

Mchezaji wa Chelsea Callum Hudson-Odoi akishangilia baada ya kufunga bao la tatu katika mechi Chelsea iliwaridima Dynamo Kyiv magoli 3-0 ugani Stamford Bridge.

Usiku wa kuamukia leo mechi za kuwania kombe la Europa League zilisakatwa katika viwanja mbalimbali. Timu ya Arsenal kutoka uingereza ilijipata matatani baada ya kuridimwa magoli 3-1 na Rennes ya Ufaransa kwenye mechi iliyochezewa ugani Roazhon Park. Arsenal walitangulia kufunga kunako dakika ya 4 kupitia mchezaji Alex Iwobi. Kitumbua cha vijana wa Unai Emery kiliingia mchanga wakati Sokratis Papastathopoulos alitimuliwa ugani kwa kucheza visivyo kunako dakika ya 41. Dakika ya 42 Rennes walipata nguvu na kupata bao la kwanza kupitia kwa mchezaji Benjamin Bourigeaud. Katika kipindi cha pili, Arsenal walionekana kulemewa na mechi na kunako dakika ya 65 Rennes wakapata bao lililotiwa kimiani na mchezaji wa Arsenal Nacho Monreal baada ya timu ya Rennes kuonyesha msukumo mkali sana uliopelekea Arsenal kujipiga goli. Masaibu ya ‘The Gunners’ yalizidi na Rennes wakatawala mchezo hadi dakika ya 88 ambapo mchezaji Ismaila Sarr alitinga goli la tatu lililowahakikishia Rennes ushindi. Sasa Arsenal watahitaji ushindi katika mechi ya marudiano ugani Emirates.

Kwingineko klabu ya Chelsea ilipata ushindi mnono baada ya kuwaridima Dynamo Kyiv mabao 3-0 katika mechi iliyosakatiwa Stamford Bridge. ‘The Blues’ walitawala mchezo na kunako dakika ya 17 Pedro Rodriguez akapachika bao la kwanza. Kipindi cha kwanza kilitamatika Chelsea wakiwa kifua mbele na kipindi cha pili kilipong’oa nanga, Dynamo Kyiv walionekana kumiliki mpira kwa dakika chache mno. Chelsea walijikwamua na kuimarisha mchezo wao na dakika ya 65 mchezaji Willian akafunga bao la pili kupitia mkwaju wa ikabu. Vijana wa Maurizio Sarri walimiliki mchezo hadi dakika za mwisho mwisho na nguvu mpya Callum Hudson-Odoi akapachika goli la tatu.

Katika matokeo mengine, Dinamo Zagreb iliwafunga Benfica 1-0 katika uwanja wa Commerzbank Arena, Eintracht Frankfurt ya Ujerumani ikatoka sare ya 0-0 na timu ya Inter kutoka Italia. Kulishuhudiwa mvua ya mabao ugani Estadio R. Sanchez wakati wenyeji Sevilla walipigana mabao 2-2 na wageni Slavia Prague. Zenit St. Petersburg ilijipata taabani wakiwa nyumbani Gazprom Arena walipolimwa magoli 3-1 na Villareal, Napoli iliwafunga Salzburg mabao 3-0 huku Valencia ikiwaridima FC Krasnodar magoli 2-1.

Mechi za marudio za kutafuta ni nani ataingia robo fainali ya kombe hili la Europa zitachezwa Alhamisi ya tarehe 14-03-2019.

Facebook Comments