Arsenal yadhalilishwa na Everton kwa kupigwa 1-0

Wachezaji wa everton wakisherehekea baada ya kuifunga Arsenal 1-0 katika mechi ya kuwania ligi kuu ya Uingereza, EPL

Kinyang’anyiro cha ni nani atamaliza nafasi ya nne bora katika ligi kuu ya Uingereza, EPL kinazidi kupamba moto huku timu za Tottenham Hotspur, Arsenal, Chelsea na Manchester United zikijitahidi kupata mwanya huo.

Tayari klabu za Liverpool na Manchester City zimejikatia tiketi ya kucheza michuano ya klabu bingwa barani Ulaya UEFA Champions huku zikihitajika timu zingine mbili kutoka Uingereza kujiunga na ‘The Reds‘ na ‘Citizens

The Gunners‘ walipata pigo hapo jana baada ya kupigwa goli 1-0 na timu ya Everton katika kipute kilichosakatiwa ugani Goodison Park, bao la vijana wa Marco Silva lilipachikwa wavuni na mchezaji Phil Jagielka kunako dakika ya 10.

Kufuatia kipigo hicho, Arsenal inasalia nafasi ya nne ikiwa na pointi 63, pointi sawia na timu ya Chelsea inayoshikilia nafasi ya tano, Tottenham Hotspur ni ya tatu na pointi 64 huku Manchester United ikiridhika na nafasi ya sita kwa kujipa pointi 61. Liverpool ndio inaongoza jedwali la ligi ya EPL ikijizolea pointi 82 baada ya kucheza mechi 33 huku Manchester City ikishikilia nafasi ya pili na pointi 80 ikiwa imesakata mechi 32.

Leo (Jumatatu) mchuano mmoja wa kuwania ligi hii ya EPL unaratibiwa kucharazwa wakati Chelsea itamkaribisha West Ham United ugani Stamford Bridge majira ya saa nne usiku (10 pm) saa za Afrika Mashariki.

JEDWALI LA EPL

Facebook Comments