Arsenal kuchuana na Manchester United Jumapili saa moja unusu ugani Emirates

Vita vya ni nani atamaliza nne bora katika ligi ya Uingereza EPL vinaendelea wikendi hii huku mechi kubwa ikiwa ni baina ya Arsenal na Manchester United ugani Emirates Stadium majira ya saa moja unusu usiku saa za Afrika mashariki. Manchester United wanaingia katika mechi hii wakiwa na morali baada ya kufuzu kwa awamu ya robo fainali za kombe la UEFA Champions kwa kuwatoa PSG katika ushindi wa goli la ugenini baada ya timu hizi mbili kufungana 3-3 kwa ujumla. Kwa upande wao Arsenal walichabangwa mabao 3-1 na timu ya Rennes katika mchuano wa Alhamisi wa kombe la UEFA Europa. Mara ya mwisho timu hizi mbili kupatana ilikuwa mwezi Januari mwaka huu wakati United ilimtoa Arsenal katika michuano ya kombe la FA kwa kumfunga magoli 3-1 mabao yaliyofungwa na wachezaji Alexis Sanchez, Jesse Lingard na Anthony Martial.

Katika mechi tano za mwisho za ligi ya EPL, Arsenal wameshinda tatu dhidi ya Southampton, Huddersfield Town na Bournemouth, wakatoka sare dhidi ya Tottenham Hotspur na kupoteza mikononi mwa Manchester City. ‘Red devils’ kwa upande wao wameshinda mechi 4 wakicheza na Southampton, Crystal Palace, Fulham na Leicester City huku wakishikwa sare moja tu na Liverpool. Kwenye msimamo wa ligi Arsenal ni ya 5 na pointi 57 huku Manchester United ikiridhika na nafasi ya 4 kwa kujizolea pointi 58, pointi moja mbele ya Arsenal.

MECHI 5 ZA MWISHO ZA EPL, ARSENAL VS MANCHESTER UNITED

‘The Gunners‘ wameshinda mechi moja pekee wakipoteza mbili huku ‘Red Devils’ wakishinda mbili na kupoteza moja. Timu hizi mbili zimetoka sare mara mbili.

MAPATANO YA TIMU HIZI 

Wamepatana mara 230 katika michuano yote huku Manchester United wakiwa kifua mbele kwa kushinda mara 97, Arsenal wamefanikiwa kushinda mara 82 huku wakitoka sare mara 51. Ushindi mkubwa ulioshuhudiwa baina ya timu hizi mbili ulitokea tarehe 28-11-2011 baada ya Manchester United kumrarua Arsenal magoli 8-2 ugani Old Trafford.

CHENYE UNAHITAJI KUJUA

Manchester United wamepata afueni baada ya kurejea kwa Paul Pogba ambaye alikuwa akitumikia marufuku. Akizungumza na wanahabari, kocha wa Red Devils Ole Gunnar Solskjaer amesema Anthony Martial, Nemanja Matic na Ander Herrera wanaeza kujumuishwa katika mechi ya jumapili. Hata hivyo, Solskjaer hajatoa habari zozote zinazowahusu wachezaji Alexis Sanchez, Jesse Lingard na Juan Mata hata baada ya Lingard kuonekana akifanya mazoezi siku ya Ijumaa.

Arsenal watakosa huduma za Lucas Torreira anayetumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu walipokuwa wakicheza na Tottenham Hotspur. Wachezaji wengine wanaotarajiwa kukosa kipute hiki ni Danny Welbeck, Rob Holding na Hector Bellerin wote wakiendelea kupata nafuu baada ya majeraha. Mkufunzi wa Arsenal Uni Emery amesema itakuwa mechi ngumu lakini watatumia mbinu zingine tofauti na zile walitumia katika mechi ya FA waliopoteza 3-1 mikononi mwa Manchester United.

Mwamuzi wa mechi hii atakuwa Jonathan Moss huku wasaidizi wake wakiwa Simon Bennett na Marc Perry, Martin Atkinson atakuwa afisa wa nne (Fourth Official).

RATIBA YA JUMAPILI, 10-03-2019

Liverpool vs Burnley saa tisa mchana (15:00)

Chelsea vs Wolverhampton saa kumi na moja na dakika tano (17:05)

Arsenal vs Manchester United saa moja unusu usiku (19:30)

Facebook Comments