Ruto ni kizuizi katika vita dhidi ya ufisadi, Kutuny asema

Siku chache baada ya naibu Rais William Ruto kusema idara ya upelelezi wa jinai, DCI inatumika vibaya na wanasiasa katika vita dhidi ya ufisadi, sasa mbunge wa Cherengany Joshua Kutuny amemkashifu Ruto kwa kukosoa idara zinazofanya uchunguzi wa mafisadi akisema Ruto ni kizuizi kwenye vita hivi.

“Wewe ni wa pili kimamlaka katika taifa la Kenya, Uhuru mwenyewe ana Imani na DCI na DPP kufanya uchunguzi, mbona wewe unakosoa? Ni nini unajua watu wengine hawajui?” amesema Kutuny.

Mbunge huyu pia amewapinga vikali wanaotaka kuwasilisha mswada bungeni kupunguza makali ya idara zinazopigana na ufisadi akisema wabunge wanapaswa kutengeneza sheria za kuongezea idara hizi nguvu.

“Sasa wamelete sheria bungeni wakitaka kupunguza makali ya DCI na DPP wasichunguze mafisadi kwa sababu wana wakora wengine wanaokula nao huko, kwanza wabunge wanapaswa kutengeneza sheria za kuongezea idara za kupambana na ufisadi nguvu ili  mafisadi wakamatwe asubuhi na saa nane mchana wafikishwe mahakamani na kushtakiwa,” Kutuny asema.

Kutuny ameendelea na kumkashifu Ruto akidai anakusanya wabunge wanaomuunga mkono wamtusi Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati uo huo, Kutuny amesema ufisadi ulitekelezwa katika ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer yaliyoko kaunti ya Elgeyo Marakwet akisema uchunguzi ushafanywa na waliohusika wanajulikana na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za sheria.

“Wizi ulifanyika katika mabwawa ya Arror na Kimwarer, uchunguzi umefanywa na kubaini bidhaa za ujenzi zilimwagwa katika maeneo yaliyotengewa ujenzi huo, sasa nauliza serikali, DPP na DCI waharakishe kuwachukulia hatua waliojihusisha na ufisadi katika ujenzi wa mabwawa hayo” amekariri mbunge huyu.

Facebook Comments